Ukweli japo mchungu, nitasema sikufichi,
Ee Mwanamoi mwenzangu, ulepita mtihani,
Kwa werevu walimwengu, ukajipisha nafasi,
Iweje uje chuoni, kisha uwe mkabila!
Tulipoingia humu, heshima lihanikiza,
Lugha lokuwa muhimu, kiswahili kiingereza,
Liiramba gani sumu, ulimi ukateleza,
Iweje uje chuoni, ukabila kueneza!
Msichana mvulana, kitaka suhubiana,
Msichana tauliza, jinalo la kikabila,
Kiwa Njeri 'we Ogola, usuhuba utaoza,
Iweje uje chuoni, ukabila kuzumbua!
Kwenye siasa za chuo, twazifanya kikabila,
Tukifanya miungano, twateua makabila,
Kura nazo za mchujo, twazipiga kikabila,
Iweje uje chuoni, ukabila kukomaza!
Najua utamaduni, lugha ndiyo mhimili,
Lakini pachagueni, siwe pa mihadharani,
Tamaduni huwa duni, wengi kiwa kizuizi,
Iweje uje chuoni, kudunisha utamaduni!
Wanasema kisokula, mlimwengu sera nale,
Ila viovu twavila, badala shetani ale,
Ukabila ni chakula, cha shetani na jinale,
Jamani si' Wanamoi, tuuwinge ukabila
No comments:
Post a Comment