Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Saturday, 25 June 2016

TANABAHI

Wagalatia 5:7'mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msitii kweli'? Mara nyingi huwa ni kutamauka. Labda ulitarajia mambo yawe bora kabisa ukiwa karibu na Yesu lakini wokovu umekoroweza hadhi yako maishani kabisa. Pia, labda jirani, rafiki au mtu yeyote yule alikushauri dhidi ya wokovu. Pia uraibu wa dhambi ulizokuwa ukifanya hapo awali umetia doa katika nguo yako ya ukristo. Mhubiri 7:14 inasema 'siku ya kufanikiwa ufurahi na siku ya mabaya,ufikiri' .inamalizia kwa kusema kuwa hayo ni 'mafumbo ya maisha'. Mstari huu unatupa taswira ya jinsi Mungu anavyofanya kazi katika maisha ya yetu. Ya kuwa, huleta siku za ufanisi ili tufurahi na pia, huleta mabaya ili tufikiri na tujitume zaidi kwake yeye. Mafumbo ya maisha ati.

Kumbuka hadithi ya mwana mpotevu. Siku zile, alipokuwa chini himaya ya babake, mambo yalikuwa mazuri. Alikula na kunywa kwa shibe yake. Lakini, chombo kilianza kwenda mrama wakati ambapo aliamua kujitenga na babake. Akauza urithi wake na kujikurupusha hadi nchi za mbali. Anasa za ulimwengu zikawa ndizo shibe yake. Akafurahisha mwili na nafsi yake nje ya himaya ya babake. Pesa zikipokwisha, bibilia inasema, bwana huyu, alitamani hata kula na nguruwe. Maisha ya pangu pakavu nitilie mchuzi yakamwanda. Lakini, siku moja alipiga moyo konde. Akafikiria. Iwapo nyumbani watumishi wa babake wanakula, kunywa na kusaza, iweje yeye ateseke. Akarudi nyumbani ili kuomba radhi kwa babake. Mafumbo ya maisha.

Hadithi hii ya mwana mpotevu inatuhimiza kuwa;hata ingawa tumemkiuka mungu na kujihusisha na dhambi nyingi,baba yetu ni yule yule; jana, leo na hata milele. Yeye ni mwepesi wa kusamehe na wakati wote, hupenda kondoo wake waliopotea warejee na hapo, atawakaribisha kama mwanampotevu alivyokaribishwa na babake. Zaburi 4:4 inasema kuwa, 'mkiwa na hofu, wala msitende dhambi. Tafakarini vitandani mwenu na mtulie'. Ikiwa basi tutahepa dhambi wakati wa majaribu, kwa kutulia na kutafakari makuu ambayo mungu amewahi kutufanyia , kama mwana mpotevu, tutarejea kwake bila hofu naye atatupokea kwa shangwe.

Hakuna mtakatifu humu duniani tangu siku za wale majagina wa imani. Mfalme Daudi, alitamani na hata akazini,lakini hilo halikutikisa imani yake kwa mwenyezi mungu. Sasa mbona wewe ufishe imani yako kwa mungu baada ya kukosa? Njoo ukamwombe msamaha.

Mkumbukeni Ayubu na mateso yake. Alifiwa na wanawe na mifugo. Akauguza maumivu mengi katika ngozi ya mwili wake. Mkewe na marafiki zake wakamshawishi amkane mungu na alitusi jina lake. Lakini la! Badala yake katika kitabu cha Ayubu 1:21, alisema kuwa, 'nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi na nitarudi huko vilevile. BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA. Jina la bwana libarikiwe'. Licha ya mateso na huzuni, Ayubu hakufa kiimani ila alimsifu mungu hata zaidi. Je, shida zako ni zaidi ya alizopitia Ayubu hadi ufe kiimani? Umefikia kiwango cha kupoteza kila kitu hadi umegeuka kinyume na amri za mungu?Zakaria 1:3,'basi uwaambie hivi, asema bwana wa majeshi, nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi'.TANABAHI. REJELEA IMANI YAKO.

No comments:

Post a Comment