Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Friday, 8 July 2016

NENO 'TUMAINI'

Kulingana na Kamusi ya kiswahili, tumaini ni matarajio ya kitu fulani au pia kutarajia uwezekano wa kufanyika kwa kitu fulani. Tumaini ni kutarajia kitu ambacho hujakiona kwa macho. Kwa hivyo, tunaweza kusema pia kuwa, tumaini ni ushuhuda wa moyoni ya kuwa, inshallah, nitakipata hiki au kile na hiki au kile kitatendeka.

Tuzamie bibilia. Ayubu akauliza katika Ayubu 17:15,tumaini langu ni nini? Na ni nani atakayeliona? Mateso, dhihaka na kejeli kutoka kwa wanadamu, chuki na hata uongozi mbaya ndivyo vyanzo vya kuibua maswali haya kwenye bongo za mwanadamu. Matatizo ya kuradidi licha ya kuishika njia ya msalaba kwa dhati. Umaskini katika familia umekuwa kibwagizo cha kila ubeti wa maisha. Ukosefu wa karo. Licha ya kujitahidi kimasomo, bado alama zako hazitoshelezi juhudi zako. Maombi! Maombi! Agano baada ya agano na mungu ila bado. Haya humkosesha mtu tumaini, ndiposa Ayubu akauliza, li wapi tumaini langu? Lakini, yafaa tufe moyo tukikumbwa na majanga? Najua wakati mwingine lisilo na budi hubidi lakini si lazima. Binadamu aliumbwa na moyo. Moyo wa hiari. 'Nifanye au nisifanye' ? Hizi ndizo sauti zinazoshindana moyoni. Chaguo, hutegemea uketo wa imani na fikira za mtenda. Na je, Mungu anatarajia nini iwapo tutakumbwa na matatizo?

Warumi 5:3-5 'wala si hivyo tu, ila mfurahi katika dhiki pia, mkijua kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi. Na kazi ya saburi ni udhabiti wa moyo, udhabiti wa moyo nao huleta tumaini. Na tumaini halitahayarishi, kwa kuwa pendo la mungu limemininiwa katika mioyo yetu na Roho mtakatifu tuliyepewa sisi'. Ni kuwa, matatizo huja ili kuimarisha imani na uvumilivu. Labda, kile ambacho unaombea ni kidogo sana na anatarajia uombe hata zaidi kwa kile ambacho moyo wako unatarajia. Au pia, labda, mustakabali (future) wako ni mkuu sana hadi mwenyezi Mungu anakupitisha kwenye haya yote, ili kukupa uvumilivu na kuimarisha imani yako kwa ajili ya lile kubwa ambalo amekuandalia. Mungu anataka tuvumilie, tuimarishe nyoyo zetu halafu baadaye, tujazwe na tumaini. Tumaini la mwumini ni kwa mwenyezi Mungu.

Wengi wetu huwa na tumaini ikiwa tutapata fununu ya kile kitu kutendeka labda kwa kuona mwanga fulani. Lakini warumi 8:24 inasema kuwa, kwa maana tuliokolewa na taraja, lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayetarajia kitu kinachoonekana? Bali tukitarajia kitu kisichoonekana, twakingoja kwa subira. Jambo jingine linajitokeza tena, Subira. Tumaini ni subira. Maombi yetu yanakawia kujibiwa ili mungu ajaribu kutathmini kina cha subira yetu kwake. Kwa kuwa, sote tunaamini kuwa, mwishowe Yesu atarejea kutuchukua lakini jua kuwa si leo, si kesho wala kesho kutwa ila atakuja kwa kuwa ujio wake, hata malaika wenyewe hawajui. Ndiposa anaimarisha subira yetu. Ili misuli yetu ijazwe nguvu na mioyo yetu ijazwe nguvu za roho ili hata akikawia sana, tumaini letu halitokufa. Hatumuoni ila tunamwamini na ndiposa tunamtumainia. Zaburi 147:11 inasema kuwa, bwana huridhia wale wamchao na kuzitarajia fadhili zake. Mungu wetu, hupenda wale wanaoyaweka matumaini yao kwake licha ya ugumu wa hali kwa utukufu wa jina lake. Fanya uamuzi leo. Kama ilivyo, IMARA YA CHOMBO NI NANGA, vivyo hivyo NANGA YA MAISHA NI TUMAINI KWA MWMKAWINI.


No comments:

Post a Comment