Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Tuesday, 5 July 2016

KASISI SIASANI!

Ikiwa wapo wanadamu wenye ulimi mwepesi ni makasisi. Ikiwa wapo waliobobea katika kukaliri na kunukuu maneno ya vifungu virefu ni makasisi. Ikiwa wapo wenye uwezo wa kuvuta mbingu na kuileta karibu na ardhi ni wale wale. Kasisi atawaongoza kondoo anaolinda na kulisha kwa nguzo mbili tu : Imani na tumaini. Atakuelezea ubora wa mbingu na kukuchorea taswira ya kiti cha enzi, malaika wanaoabudu na pia kitabu au buku la hukumu liliojazwa makosa ya kila mmoja. Baada ya ganga ganga zote hizo, muumini hubaki akitabasamu na kuapa kufuata aliyoambiwa. Bila kujali uamuzi wa muumini, kasisi huyo, na kikapu chake. Anakusanya sadaka za kuendeleza uinjilisti. SADAKA. 

Inashangaza sana kuwaona baadhi ya wanasiasa ambao kazi yao ni;ahadi. 'mkinipa kura, nitajenga safina ambayo kila mtu atutumia kuvuka hadi ng'ambo ya pili bila malipo! Nitajenga zizi kubwa ambalo, enyi nyote mlioelemewa na mizigo mizito, mtakaa mle na kustarehe'. Unaahidiwa zizi, na sisi vipofu, tunakubali kwa kauli moja, 'naam! Wewe ni baba,baba yetu! Wewe ni mama yao'! Huku tumesahau kuwa, tukiwa zizini, kwanza tutafugwa kama ng'ombe ;ukiwa mwanamume, aidha utahasiwa na kufanywa gari dogo linalotumia damu badala ya mafuta au, utakuwa kijalizo cha haja za mkubwa wako. Ukiwa wa kike, utakamuliwa hadi usinyee au pia, si unajua siku hizi pia ng'ombe hufanywa wake za wahuni! Bora ukubali kuishi zizini. Bila kusahau kisonzi. Ole wetu. 

Siasa inasemekana ni mchezo mchafu.Muradi wewe ni Mwanasiasa, unahusishwa na zile sifa mbaya; Mpyaro, kitimbakwiri, mtoa kadhongo, mkorofi, mshirikina na wakati mwingine, wengine huwa wahafidhina, hawakubali mabadikiko ya aina yeyote. Sifa hizi, pamoja na uhasama unaojitokeza kati ya mwanamalevya na mwanamalegeza katika uwanja huu, zinachangia mchezo huu kupagazwa uchafu. Miongoni mwa mahasimu;tende, tendeje! Nyama nyamaa! Pembe kipembe ndiyo kauli yao mbiu. Lakini umegundua kuwa toma na toma hazitomani na ndovu wawili wakipigana, ni sisi ndio tunaoumia! 

Zamani, mtu aliingia kwenye siasa kwa nia ya kutafuta suluhu ya jambo fulani ambalo anahisi watangulizi hawajaliwajibikia. Na ndiyo maana vyuoni, viongozi waliochaguliwa siyo kwa misingi ya kikabila, rangi, dini wala miungano, ila sera zake ndizo zilizomnadi. Mgombea hakuhitajika kuwanunulia wapiga kura chai, au kuwapeleka hotelini wale ugali mix ndiposa wakawapigie kura. Kazi ya kasisi haikuwa kununua washiriki wengi ili apanue jukwaa lake la kukusanya sadaka nyingi. Hawakuhitaji kufanya miujiza mingi ambayo usuli wa nguvu zake ni tashtiti, ili kuwavutia watu. Mwingiliano wa maneno na bibilia, na ambayo yanahusu swala fulani ibuka yaliuza jina lake. Jambo la hisani ambalo amefanyia jamii kwa takrima, hata likiwa dogo lilinadi jina. Hizo ni zama zile, za chanjagaa aliyejenga nyumba akakaa. Zama za howe ni kwa wafumao. Siku hizi kuna howe? 

Hongo imehanikiza kote. Panda mbegu. Shamba halijulikani. Siasani, hawauzi sera bali sura huuzwa. Ukiwa na pesa, hata ikiwa huna kinywa cha kushawishi,wewe ni wa kila mtu. Ukiwa na uwezo wa kunena kikabila, utakuwa kama duma, ukitoka hutakosa windo. Siku hizi, pesa zina utukufu kuliko mkawani. Zina uwezo wa kuumba na kuumbua. Iwe maabadini au siasani. Makasisi wa, mwenye kisu kikali, ndiye alaye nyama. 

No comments:

Post a Comment