Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Saturday, 20 August 2016

MATIANG'I KASOME HAYA



Wanasema waneni kuwa elimu haina mwisho. Ni kweli kwamba binadamu haiachi elimu hata akiwa kaburini kwani huko,hujifundisha jinsi ya kuwa mpweke,kupambana na joto na mafunza makubwa makubwa na kuishi gizani. Elimu ni kweli haina mwisho kwani katika kila hatua anayopiga binadamu, kutoka tumboni mwa mamake,akaja duniani kwa kilio cha kubadilika kwa mazingira,akakuzwa kwenye maisha ya tamu chungu hadi kufikia kiwango cha kuolewa au kuoa. Hapo akarambishwa asali na shubiri ya maisha ya ndoa. Katika hatua zote hizo,binadamu huyu hujifunza jinsi ya kupeta mtama na kutenganisha mchele na dume ili angalau ajisawazishe na maisha ya humu duniani. Anajielimisha. Lakini hiyo ni elimu inayofungamana na methali ya elimu maisha si vitabu. Elimumaisha ambayo mtu hahitaji kutahiniwa darasani na matokeo yake kupewa. Elimumaisha ni ile inayohitaji uelekezi na matokeo yake mara nyingi hutegemea mtazamo wa mtu binafsi kimaisha. Elimumaisha haina mwisho. Lakini elimu vitabu je!
Hadhi ya masomo humu nchini inaendelea kudidimia na karibuni yataonekana kama ‘zilizopendwa’ kutokana na mkondo ambao elimu ya vitabu imechukua. Tuanzie kule chini ambapo wanafunzi wengi hupewa mafundisho yanayolenga kupita mtihani bali si kuoanisha ajifunzayo yeye na mazingira ya kihalisia. Kwa mtazamo huu,mwanafunzi hubeba ile dhana ya kupasi mtihani hadi shule za upili. Elimumaisha hujichopeka ndani kutokana na mabadiliko ya mazingira ambapo badala ya mwanafunzi kuchagua majibu kama ilivyokuwa awali, inampasa ajieleze moja kwa moja. Hapa,elimumaisha huchuja tiara na ndege. Na mara nyingi,kwa kuwa wengi huazimia kuwa ndege,watatumia mbinu zote ili kuhakikisha kuwa jongoo anapanda mtungi. Wizi wa mtihani huchukua nafasi kubwa katika akili za mwanafunzi. Ajabu ni kuwa walimu pia husaidia katika vitendo hivi haramu kwa kisingizio cha; huenda mtama mui,wapishi pia wakatwikwa ubaya. Hapa elimu vitabu,shabaha yake kuu hubadilishwa na kumfanya  mtu aasi mipaka ya elimumaisha na kumfanya awe mwewe wa kuotea vifaranga kwa jicho lake kali hata akiwa amefukiwa kwa mavumbi kule angani. Muradi mwenye kuku awe amezubaa au hayupo kabisa. Mwalimu naye hutoa machozi ya mamba au tuseme huwa jogoo wa ‘uta wangu u kuleee’ ilhali bayana anaifahamu.
Kwa kujaribu kuoanisha mwanga na giza,wanafunzi hawa hujipata vyuoni wakifanya kozi ambazo alama zao zinawaruhusu ila ndani moyoni,wao hujua kuwa asilani, ng’ombe hawi mbogo. Hili husababisha kubadilisha kozi na ambapo kozi zinazositiri manusura wa kwingineko ni zile zinazohusisha elimu na ualimu kwa jumla.
Mambo yakiwa msagunda mara tena,mtindo wa kula ugali kwa uma au niseme kumeza vidonge vya dawa kwa sharubati huendelea badala ya maji kulingana na masharti ya mganga. Kwa kuogopa kunawa mikono, labda kwa uzembe,woga wa maji au hata kuona kuwa ni kupoteza muda huko,ulama huchukua uma kwa jina ‘mwakenya/ndula’ na kuitumia kula ugali ambao kwa shibe kamili,ya kweli na inayojulikana kwa wafrika wengi,ni lazima ule kwa kuumega kwa viganja. Baadaye,wao huhitimu na kuingia katika uwanja wa kusaka kazi.
Fikiria basi wafanyakazi ambao wataajiriwa baada ya tamthilia ya wizi kutoka mimba kupasuka hadi kumaliza chuo kikuu. Fikiria utendakazi wao. Fikiria kuhusu mwalimu ambaye alipitia katika njia hizo zote na akaajiriwa na serikali kuja kumfunza mwanao. Atakuwa kielelzo kipi kwa atifali! Ikiwa gunia la chumvi hurishai chumvi,basi usishangae kizazi kijacho kikiwa vile vile hadi ujio wa yesu mnazareti. Zingatia Yule daktari wa karne ya ishirini na moja. Hajali uzima wa mtu,hajali dhamani yake kwa nchi. Ameuzika utu kwenye kaburi na kulitandazia zege. Kwake,maisha na matibabu si haki kwa makabwela. Pesa bora. Fikiria kuhusu mhandisi yule,labda ndiyo sababu ya kupenda sana wachina na wajapani kwa kuwa labda mpanda hila,ni sharti avune ufukara.
Ukimpata matiang’i mwambie,
Mtoto memnyang’anya kisuche,
Hata banzi asimpe
Kampokeze ombwe……labda hilo litafanya mti ufe,shinale na tanzuze zikauke.

No comments:

Post a Comment