Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Sunday, 4 September 2016

HUBA NDULI

Kawaida ugonjwa ni hali ya mwili na viungo vyake kutofanya kazi kwa njia ya kawaida.Ugonjwa wowote huwa na kiini ambacho huwa ni uchafu ambao binadamu huingiza mwilini kwa hiari au bila hiari. Lakini kwa weledi wa wanasayansi, kupitia kwa waganga magonjwa mengi hutiba ila mengine hayatibiki isipokuwa kwa imani ya kidini.  Lakini kuna gonjwa ambalo ukiugua,wanasayansi hawana nguvu za kuutibu wala kutafuta dawa ya kupunguza makali yake. Gonjwa hili hutokea kati ya watu wa jinsia tofauti ambao huingia mkataba wa usuhuba kati yao. Zimenitikisa leo nizungumzie dalili za mwisho wa huba. Huba,ambao ni ugonjwa usiobagua umri kwani pia,paka mzee eti hunywa maziwa.

yakichipuka
yakichipuka mapenzi huwa kama ndoto. Yakichipuka,wanagenzi wawili hujiona katika anga ambayo hawana dhana   ya kuwa wataiondoka. Wawili hawa huyaona maisha yao kama udhanaishi ambao si kila binadamu huweza kuwamo. Mwanamume humwona wa kike kama barafu ndani ya jokofu,nyeupe mithili ya dheluji na inayotakiwa kutunzwa kama yai. Mwanamke naye humwona mume kama gunia la dhahabu linalorishai huba la kweli. Yakiwayeyusha,wao huyaona mapenzi kama umande ambao humezwi na miyale yajua.


Kwa hatua
Kwa hatua mapenzi yenyewe hukua kutoka kiwango kimoja hadi kingine. Wasemavyo,huba ni kama mgomba ambao ukipandwa,kama mimea mingine lazimna ukue. Kwa hatua,kila mtu hupata kujua siri zilizobanwa katika moyo wa mwenziwe. Ahadi nyingi huwa kama chumvi katika maji ya bahari,maji yaliyojaa huba ambayo hawa wawili huogelea. Kama vipofu,wawili hawa huongozana na kuliona baya la mwenza kama heri. Kama kiziwi,maneno yote asemayo mwenza hayasikiki ila kwa kitapo cha moyo,humaizi kuwa amenena ya kheri. Yakiwa ya kweli,hata hadhi ya mfuko huwa si hoja tena. Mkorowezo wa sura huwa si hoja tena. Aghalabu wawili hawa hujiona kama waamba ngoma wawili walioketi upande mmoja na wanaovuta ngozi moja kumoja. Wote,huvuta kwa upande mmoja,wao. Yakiwayeyusha,wao huyaona mapenzi kama bahari ambayo wataiogelea milele.


Kwenye kilelecha
Kwenye kilelecha mapenzi huwa sasa kama mpira wa kandanda uwanjani. Kila mchezaji huutafuta mpira huo ili angalau asiwe wa kulaumiwa kwa kufifia kwa timu. Weledi zaidi huuchukua mpira na kuupaka mafuta kusudi afurahishe mashabiki na watazamaji. Wale wa wastani hucheza tu kusudi wenzake wamwone kuwa hajaijaza nafasi tu. Mwenye huba la kweli,hucheza kwa namna ya kumfurahisha yule mwenzake. Kwa kumpa pasi nzuri,kumpa moyo akiteguka na kushabikia juhudi zozote afanyazo hata zikiwa za kuijifunga bao kwani bao ati ni part of the game. Yakiwayeyusha ,wao huona mapenzi kama mpira ambao japo ni mzito,ni mtamu wakati mwingine. Panda-shuka eti.


Yakizidi sana
Mapenzi si kama ngoma,yakizidi ,humjukumisha mhusika mkuu zaidi. Mwenye stahamala mara nyingi huumia kwani huegemezwa uzito zaidi. Huu ndiyo wakati ambapo kidole kimoja kina uwezo wa kumwua chawa. Hapa,kofi hulia kwa kiganja kimoja na jifya moja moja huinjika chungu. Maajabu ambayo hutokea tu kwa yule mwenye imani na tumaini la dhati. Mwenye kasi ya kushindana na hewa. Atapiga simu yeye tu! Atatuma arafa ya heri au ‘umeamkaje na njozi njema’ yeye tu. Siku zote ndiye mwenye kusema ‘ninakupenda’ilhali mwenziwe kazi yake ni ‘pia’.  Yakikengeuka,barafu huanza kuyeyuka,gunia la dhahabu huanza kuwa gunia la mkaa,chafu kuzidi kipimo. Umande,huanza kuwa na uhalisia.


Yakimwagika
Yakimwagika yamemwagika. Mwenye mali ya chuki na maneno ya nyoka,huchiriza sumu ya swila. Mwenye roho ya shashi huchukua kamba na kutia shingoni asimwone tena mtesi wake. Mwenye kutataga akili, huchukua gongo au mtungi wa pombe na kufanya kileo kuwa mate yake ya kila wakati kusudi asimkumbuke. Wa ngeu nyeusi huchukua upanga na  kutenga mwenzake na uhai. Ilhali mwenye moyo wa tumaini,hujuwa kuwa mlango huu ukifungwa, mwingine hufunguliwa hata ikiwa ni baada ya muda kwani yu wapi mtesi atasaye milele? Yakikengeuka,mapenzi hukosa mbolea na kama mgomba,husinyaa yasizae ndoa au hunyauka na kufa kama ua.

 AMA KWELI YANATATIZA,NINGEKUWA NA NJIWA…………………..NINGEMFUMBATA NJIWA,NIMPAKATE…………….NA BAADAYE…….TUOMBEANE HERI                        

No comments:

Post a Comment