Nilikuona mkutanoni umeketi na Kipungu. Mlikuwa katika hoteli ya kifahari, kubwa kabisa kwenye katika kaunti yetu. Lililowaleta pamoja si kingine, ila Kipungu anakushawishi uende utahadharishe kuku wenzako kuwa ni lazima wasakure na kupata wembe kwa muda ufaao. Kipungu anasema kuwa kuku wenzako wamekawia sana kuupata wembe. Unapewa shilingi hamsini na vijikaratasi vya vitisho. Vitisho kwa kuku wenzako. Huyo mnaachana na Kipungu katika hoteli hiyo, unaenda kwako madongoporomoko naye anaekekea kwake kwenye mtaa wa kifahari. Nani mwenye akili, mchochezi au mchochewa? Ningekuwa wewe, ningejua kuwa vitisho hivyo vya kutafuta wembe, pia vinanihusu. Kwani miye pia ni kuku ambaye anatahadharishwa. Lakini shida ni kuwa eti wewe ni jogoo. Nikukumbushe, kipungu akija kuwala, hatachagua wa kumla, wewe au wanao pia watakuamo. Kuku ni kuku, JOGOO NI JINA TU!
Ulikuja ukatuzomea sana huku madongaporomoko. Ukasema kuwa ni lazima tumsaidie Kipungu kutafuta wembe wake. Ati alikuwa mtini, yeye na mwenzake waking'ang'ania wembe. Ukawaponya wembe huo na kuanguka ardhini. Lakini si unajua yeye huruka angani, ati kusakura mchangani atachafuka. Makucha yake ni kurarua si kuchakura. Ati, kuku ndiyo wasakuraji. Alikutuma awali tutafute ila hatukupata. Ndiposa sasa anakutuma mara ya taru hii. Ukaja na vitisho vingi ajabu. Ukatutia baridi sisi makabwela. Lakini nakushangaa. Mbona unatumiwa kututisha, sisi kuku wenzako, makabwela wenzako na jirani zako katika kijiji cha madongonporomoko?
Siku ngapi sasa zimeisha hatujapata wembe. Ulikwenda kwa Kipungu tena. Mara hii hakukuonya hata kidogo. Ila kakupa ukamba, uje umfunge kila kuku mguu na umwanike nje uwanjani. Angalia vifaranga wa wenzako wanalia, husikii. Ona kuku wenzako wanakuusia husikii. Unafanya kazi uliopewa na bwana. Punde kipungu anakuja na wenzake. Wanaanza kumbeba mmija mmoja wale uliowafunga nje. Vifaranga wa wenzako wanalia wakiwa kati ya makucha ya kipungu, mwako kizimbani unacheka tu. Hatimaye wanaliwa na kumalizwa.
Unaitwa tena. Unapewa mpynga na kuambiwa uende uwalishie vifaranga wako. Umwagapo nje, Vipungu ambao wamejibanza mitini wanawabeba wanao wote. Jamii yako inaisha sasa. Umesalia pekee. Jioni ya kesho nasikia wataja kukuchukua nawe pia. Ulijifanya Jogoo, nikakwambia usijione kipungu kwa kuketi nao kwenye meza moja. Unakishwa maneno ya kuchochoe na huoni? Kumbuka kipungu hula nyama freshi, wewe kuku hukosa hadi kula kinyesi. Paka mnono si Chui, Mbwa mnono si Simba, panzi kati ya nzige si Nzige. Kipungu anapaa angani, akitengeneza makucha yake huku wewe sasa unachakura pipani ukitafuta angalau kinyesi ule. KUKU NI KUKU, JOGOO NI JINA.

No comments:
Post a Comment