NINAZIKWA NINGALI HAI
Jeneza nakuona, nakufikiria, nakuhisi, ninainusa harufu yako mbaya kama panya anayeoza. Unanikodolea macho pima kana kwamba ninakuchelewesha. Najua unanisubiri sana nije unilaki, nilale kwako nikisafirishwa katika ulimwengu wa pili. Wanasema ulimwengu wa kiroho. Lakini nikuulize, unafikiri kwa miaka yangu hii sabini duniani niko tayari kufa? Najua wewe hubishi wala kupeana taarifa kwa kuwa sote tungekutoroka au wenye misuli wakukabili wakuue badala ya wewe kuwaua wengine, lakini hilo halitoshi kunikodolea macho kila wakati. Zamani nilidhani ulijengewa wazee wakongwe ambao wamebugia chumvi si haba, kumbe hapana. Siku hizi hata vichekechea wavichukua tu. Unawaliza mama zao. Najua utapinga ila nikukumbushe. Unamkumbuka Kwekwe Mwandaza? Unamkumbuka Samantha Pendo? Wote hawa waliuawa kwa ajili ya amri yako. Uliamrisha polisi atumie mtutu wake bila uangalifu wowote.
Polisi siku hizi. Zamani ulitumia makundi ya haramu. Nikutajie Sungusungu, Chinkororo na Amachuma kutoka Kisii. Nikutajie Mungiki kutoka eneo la Kati, nikutajie Sabaot Land Defense force kutoka Mlima Elgon, Nikutajie Taliban na The Bangladesh Boys of Kisumu. Usisahau Kaya bombo Raiders na The forty brothers.
Kisha hukushiba uliposababisha The Garbatulla massacre na kumeza nyoyo 2,700? Hakutosheka na mauaji ya Wagalla mwaka wa 1948? Halafu juzi, mwaka wa 2008 ulipomeza zaidi ya nyoyo 1,300 wakiwemo watu waliouliwa katika kanisa la Kiambaa? Hushibi jeneza? Bado unataka kumeza. Angalia unavyowazungusha watu wanaowafuata wanasiasa. Ati unasema wenyewe wanakuita? Lakini si wanapigania haki yao kidemkokrasia. Najua hii ni Afrika Jeneza, lakini usituangamize. Wewe unatujua vyema na siku zote, likujualo halikuli likakumaliza.
Halafu nakushangaa sana. Wanaokutengeneza hawakutumii. Naona unacheka eti hicho ni kitendawili. Mimi sicheki. Naugua, napelekwa hospitalini lakini langoni nakuoni umeketi. Umepanua kinywa tayari kunikaribisha. Huoni kama huko ni kunikatisha tamaa mimi mgonjwa? Nakusihi, ondoka kwenye lango la hospitali ili gangaganga za Mganga zilete tumaini. Unawakatisha tamaa maututi kuniliko.
Wengi wanakurembesha. Wanakuwekea kisalaba kwa maana ya 'promotion to glory' hata kama unasafirisha mchawi au muuaji mwenzako. Wengine wanakutengeneza kwa dhahabu hata ikiwa atakayekutumia ni sawa na gogo linaloelea katikati ya bahari. Wengi wanakutengeneza kutoka kwa mbao za miti, mbao ambazo zingetumika kimtengenezea unayesafirisha kitanda kizuri ili asiumwe na nyoka aliyesababisha mauti yake na miti ambayo ingetumika kama fito za kuezeka nyumba yangu vyema kabla haijaniangukia na kuniua. Aidha mchoyo ni wewe, au mnunuzi, au mtengenezaji kwa kuwa ninayesafiri nitafika nikwendako hata nikitupwa uchi kaburini.
Nitazame nakulilia. Ewe Kenya jeneza la mauti. Ikiwa si polisi kumwua raia, basi ni Alshabaab kumwua raia na polisi. Ikiwa si ajali kule Salgaa, basi ni wizi wa ng'ombe kule pokot magharibi. Ikiwa mkubwa hanunui uhai wa mkubwa mwenzake, basi cancer inamnyakua mkubwa na kumsafirisha ahera. Kenya inameza Nguzo kuu za familia nyingi. Jeneza hili linameza tumaini la mabadiliko. Mbona uwe hivi ewe jeneza? Mbona uruhusu mnyama kumla mwenzake kwa sababu ya siasa? Mbona polisi atumie risasi yake ovyo? Kenya, ningesema sikupendi tena, ila sina nchi nyingine mfano wako. Wacha nivumilie jenezani. Nazikwa ningali hai.

No comments:
Post a Comment