Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Saturday, 2 December 2017

JENEZA LA MAUTI 2

NINAKUTUMA KAULENI

Hili jani ninakupa Kauleni. Ulishike vizuri usiliangushe njiani. Ni lenye umuhimu mkubwa kwa wazalendo wa nchi. Wale wanaolia machozi wakisikia mitutu ikihaniza hewani. Wale wanaohuzunika nyoyoni wakiwaona wenzao wakiangamizwa kwa ujeuri wa mianzi ya bunduki. Wanaulizana ; mbona iwaendee wapanzi bali si wajenzi? Mianzi isiyobagua umri, hata vijusi, inaruhusu risasi kuviokota. Wazalendo, wenye nchi wanalia. Ndiposa ninakupa jani hili.

Ukifika Kauleni, wambie utakaowapa kuwa kamwe si kuti kavu. Hata ikiwa ni jani tu, walikubali na wasikie maneno utakayowaambieni kwa niaba yatu.

Ukifika, anza hivi. "sisi wapanzi wa miti tunachoka. Tuliharibu nguvu zetu awali tukalima shamba, tukapanda mbegu zilizogeuka na kuwa miche. Miche ilipogeuka miti, mkaja mkaikata miti hiyo. Zama hizo, mlituhadaa kuwa mwaenda kutujengea safina. Safina itakayostahimili mawimbi ya ukabila, utabaka na mapendeleo. Mkatujaza imani kuwa safinani, tutakuwa salama. Hakutakuwa na Bwana wala Juma kitwana. Kumbe zilikuwa hadaa. Mlipaka tu mafupa kwenye mgongo wa chupa. Mlikwenda na kile ambacho sitapinga ni kuwa, mbao zenyewe mlitumia, ndiyo! Mlijengea. Lakini mlichojenga si safina. Mlitujengea lakini si safina, ni jeneza. Upande wa ndani mkalipaka rangi nyeupe ati kuashiria amani. Nje, chini mkapaka nyekundu eti ni damu ya waliotupigania uhuru. Kati mkapaka rangi ya kijani, ati kwa vile sisi ni wapanzi wa miti na juu kwenye 'kifunuko' mkapaka weusi ati ni rangi yetu. Kile ambacho mlisahau, ni kutupa ufafanuzi kuhusu watakaokaa ndani. Ni sote, Bwana, au Juma vitwana? Ingawa kwa sasa ninajua kuwa ni juma vitwana. Kisa ni kuwa, mitutu iliapo, hamfikiwi na risasi hata ikiwa nyie ndiyo mliosema tukusanyike tufanye Vurumai barabarani. Ati tupiganie haki na uhuru wetu ingawa ninajua kuu ni kuwa, twawapigania nyie mabwana mpande jukwaani muibe mchana hata ikiwa weusi wetu mchana unaonekana zaidi. Hamjali. Nyie ni sawa na izraili ambao hawajali wakati wa kuiba uhai wa mja.

Mbona nyinyi mabwana, tuwapo jenezani, nyie mnasimama kando mkitoa machozi ya mamba? Au kwenu huko ndiko kuomboleza? Nyie mnajua kuwa katika jeneza mlilotutengenezea badala ta Safina, mitutu haibagui umri ila inabagua tabaka na kabila. Mngekuwa werevu, badala ya kutoa vichozi wakati siye tumelala chali  jenezani bila hewa, mngetuepishia hatari hii ya mitutu. Mtatue matatizo yenu kiungwana na mtujie kutwambia mliloafikiana na lililokataa kutika. Tunajua nyie mabwana mna njaa ya kuongoza, kupata umarufu, kuishi maisha ya starehe na kama kawaida jenezani, Kuiba. Au mmejaa umero wa hayawani aidha.

Wapanzi tumechoka. Tunasikia kuwa mna mpango wa kuligawanya jeneza lenyewe mara mbili ili wengine wenu mkate kiu na tamaa ya kuongoza. Si wazo baya ila ninawashauri kuwa, ikiwa mnataka hivyo, basi nasi tupewe mbao zetu tuzipikie kama kuni. Nyie mpande miti yenu, ikikua, mtengeneze jeneza kila mmoja lake na myaweke hadharani. Kila mpanzi apendaye, aingie kwa lolote linalompendeza. Wajenzi nyie mnatuua. Mmekuwa Jogoo ambao badala ya kukabikiana na mwewe, analia 'uta wangu u kulee!' wakati vifaranga wanaisha.

Aah wajenzi. Mbona mkatujengea jeneza hili la mauti? Kisha mnalifunika gubigubi kwa kimbaa mkiitacho bendera. Kitambaa chenyewe chapendeza kweli. Lakini mbona mnatumia sahani ya chakula, kufunikia kinyesi badala ya kukitupa msalani! Jani hili ninakupa mimi Kauleni. Likutahadharisheni kuwa tunachoka na karibuni tutawacha kupanda miti au tukipanda, hatutawauzieni mjapo baada ya miaka mitano ya KUIBA bila ukomo. Ingawa kwa jina langu Kauleni, ukinipa nile nitanyamaza kwa kuwa hiyo ndiyo desturi humu mwetu." TUNAPANDA SIYE WAPANZI, MWATUJENGEA JENEZA LA MAUTI NYIE WAJENZI...AKHH! WACHA BWANA

No comments:

Post a Comment