Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Friday, 29 July 2016

KWA MUME NI JICHO

Ni kweli kuwa mungu alimpa binadamu jicho ili aweze kuufaidi mwangaza wowote ule :uwe wa jua, kurunzi au taa. Bora mwangaza. Humo, aliweka mboni, kiini cha jicho kwani huakisi mwangaza na umbo lionekenalo mbele ya mwangaza. Jicho ni la kuona. Lakini wajua macho haya ni udhaifu mkubwa kwa mume. Zimenishika leo nizungumzie yanayotusibu.

Ukimfika
Ukimfika mwangaza jichoni na mbele yake lipo umbo la mke. Mwanamume huchunguza, umbo, mwendo, mavazi, rangi ya ngozi, uzingo wa mdomo, mpepeso wa macho, mtindo wa kusuka nywele na hata urefu. Hapo, mwanamume ananasika kiakili. Anaanza kujisogeza, ulipo ulimbo. Zikimshika, huhisi kuwa ni lazima anene jambo.

Akizitwaa
Akizitwaa sifa za mke akilini. Mwanamume huanza kuwaza. Humjaji kama hakimu kortini. Hudondoa sifa nzuri na hasi. Huweka kwenye kipimo na kuchunguza uzito ulipo. Umbo : namba nane, Rangi : maji ya kunde, Kifua : cha miba, nywele : shungi la mkia wa farasi, mwendo : gari moshi kwenye reli.... Ama umbo : nambari moja! Rangi : mkaa! Kifua : mtungi wa gesi! Nywele : kidazi cha mzee! Mwendo : gari la miraa!. Huamua moyoni. Zikimshika, huhisi mtweto au mshtuko wa moyo.

Alipendezwa
Akipendezwa na wa kike, hunyatia pole pole. kama kinyonga ndiyo mwendowe. Kama njiwa, huvuta upole usoni. Kama chiriku, hulainisha sauti yake. Hata ikiwa amevaa mararuraru, hujishajiisha kama mjusi. Kama loma hupiga mbizi ardhini, kiini kikadhihirika. Kama kinyonga, hujibadilisha ili ayaafiki mazingira. Zikimshika, hujiona kama duma, akihemera, hurejea na windo.

Akimfikia
Akimfikia huanza kwa neno. Hujambo! Kisha neno hualika maneno. Ninaitwa simiyu, wewe je? Nayo maneno yakaunda sentensi. Naomba unipe sikio lako japo kwa sekunde sitini, usikie nitakayosema na usikarike nimalizapo tafadhali. Sentensi huwa aya, aya za sifa kimaumbile, kitabia na hata kiunadhifu. Sifa zenye nia ya kumchachawiza, achachawe kwa utamu wa maneno. Zikimshika, huweza kutoa hata neno siri la kadi ya ATM

Akikubalika
Akikubalika hufurahi. Akajishaua kwa wenzake. Atachukua zake picha, fesibuku ataangika. Akiwa yeye wa nia yake, huekeza na wake moyo. Mwishowe yakichujuka hukimbiana kama giza na mwanga. Zikimshika, humgeuza na kumfanya kitoweo.

Akikataliwa
Akikataliwa husisitiza. Hukunja sura akawa kama mbogo. Hujizatiti ili kudhihirisha unyamaume wake. Pia, huzingatia vicheko na mabezo kutoka kwa rafikize. Akishindwa sana, hujishajiisha kwa; bahari ina samaki wengi, hiki kidagaa hakitanifanya nipoteze muda mwingi. Kisa cha sungura kukosa zabibu. Zikimshika, humwachia matusi. Mpyaro wa kupindukia.

Jicho
Jicho la mume ni kali. Tulifananishe na lile la mwewe. Akiazimia kutafuta, hatachoka hadi apate, hata kile kilichojificha kwenye kikopesa. Chunga lisikuone ewe msichana. Kwa kuwa atakufuata kama sururu. Atakukatia ulimi wake wote. Atakuchujua, akuzuzue na azumbue penzi lililojificha moyoni mwako. Mwanzo wa safari hiyo ni jicho la mume. Zikimshika........ WASALAM

No comments:

Post a Comment