Kwa muda mrefu sana makomredi wa chuo kikuu cha hawajapata kuona raha ya wadhifa wa mkurugenzi wa burudani na mawasiliano kwenye uongozi wa MUSO. Wadhifa huo umekuwa kama mangati barabarani. Viongozi ambao hupewa wadhifa huo hujikita katika maswala ya kuandaa dundaa na kusahau mengine kana kwamba katiba imewapa wajibu huo pekee. Ndiposa, wengi wa makomredi hutegemea simu, vipatakilishi vyao au hata kwenda kwenye mikahawa kule steji ili angalau wapate habari za matukio nchini na kimataifa. Ndiposa, ninachukua fursa hii, kwa upekee na ukakawana kumdokezea mkurugenzi wetu : Bwana Dukakis Balyachi.
Julai 15,makomredi walimiminika katika ukumbi wa Student's center kwa ajili ya kupiga kura. Kwa yakini, wengi wao walikuchagua wewe Bwana Dukakis Balyachi kati ya halaiki ya wagombea waliokuwa kwenye karatasi hiyo ya uchaguzi. Waliamua kuegemeza mzigo wao kwako ili angalau uhisi uzito wanaopitia kwa ajili ya kulipia vitu ambavyo chuo kupitia kwa MUSO kina uwezo wa kuvitoa bila malipo. Kumbuka watangulizi wako walikuwa wanamonge wali kwao na mchanga wangalile kwa ajili ya kuwapa mgongo makomredi kwa kwaanika juani, kuwatembeza kwenye mvua na matope ili wapate burudani kwingineko. Kwa taadhima, huu ni ujumbe kutoka kwangu kama komredi :
Dukakis, una mwao kuwa komredi ana haki ya kupata habari,ziwe kutoka chuoni au nje ya chuo? Ikiwa umesahau mbinu za kupokea habari, wacha nikukumbushe : kuna redio, televisheni, gazeti, mtandao na hata vyama vya uchapishaji. Tuangazie hasa televisheni na gazeti mwanzo. Natumai wakati, kabla ya uchaguzi wako, ulikuwa ukiona yaliyokuwa yakifanyika kwenye ukumbi wa student's center. Makomredi hubanana pamoja kama ndizi kwenye mkungu huku wamegogomeza macho yao kwenye runinga moja. Ikiwa ni mchezo wa soka, wengine hulazimika kunyoosha miili yao kila mara kwa muda wa dakika tisini ili angalau waone pasi ya OZIL au vimbwanga vya RONALDO. Umeyashuhudia hayo? Unaamnini kwamba ni vyema komredi kupitia hayo mateso yote ilhali ana mtu wa kumwakilisha kwenye MUSO? Nenda maktabani, kuna kijisehemu kilichoandikwa Newspaper section. Hapo ndipo yafaa wapate taarifa kutoka katika magaziti yote nchini. Yapo kweli? Magazeti yamekuwa ghali hata kwa chuo jamani Bwana mkurugenzi. Eneo hilo siku hizi ni la kudurusia mabuku tu kwani kupatikana kwa gazeti humo hata kwa bahati tu, ni kama kumwona malaika Gabriel.
Unafahamu kuwa vipo vyama vya kuchapisha makala na taarifa humu chuoni! Vipo vingi tu vilivyosajiliwa lakini ni vichache ndivyo hudumisha hadho yao. Orodha ya vichache nijuavyo ni kama The Legacy, The 3rd eye, Communicator, Dafina lugha, Campus Glory, Psyche, Horizon na vingine. Vyama vingi vimefifia kwa ajili ya kukosa hela labda au kwa sababu ambazo sitazitaja kinaganaga. The informer ni mfano tu. Ikiwa basi unadhamini komredi na unajua ana haki ya kupata habari, mbona usisaidie vyama hivi kuwa dhabiti ili vimfahamishe yanayotendeka!
Wanafunzi wanaotaalumia uwanahabari wanapita changamoto kubwa sana. Tembelea kituo cha redio cha MU FM kisha ujionee uozo ulio kule. Hata ikiwa labda katiba haikupi ruhusa ya kuzama mpaka kule, una uwezo wa kushawishi uongozi wa chuo kwa usaidizi wa Mhariri mkuu ili matatizo haya yasuluhishwe.
Mwisho bwana mkurugenzi, mtu huchongewa na ulimi wake. Kumbuka ahadi zako. Msimu wa ligi za ulaya umekeribia, jaribu kukarabati televisheni au hata uongeze idadi yazo ili mwanamoi ajivunie uongozi wako. Mshoni hachagui nguo, sawazisha utendakazi wako, siasa za KALE-LUYHA na UBUNTU ziliisha. Chondechonde mpe komredi burudani. DHUKURU.
No comments:
Post a Comment