Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Wednesday, 18 October 2017

BABA AKISEMA SIPINGI!



Amani ni jambo la muhimu sana katika taifa lolote lile. Amani ni kuweza kuishi na kukaa bila shinikizo lolote iwe katika mazingira ya kiakili au mazingira ya nje. Nchi yenye amani ni ile ambayo wananchi wake wanaishi bila wasiwasi wowote wa kushambuliwa kisosholojia wala kisaikolojia. Amani ya nchi siyo kuwa na barabara nzuri za kuvutia ilhali watu wanaogopa kuzitumia kwa kuhofia maisha yao. Amani ya nchi siyo kuwa na majumba marefu mithili ya mnara wa babeli ilhali biashara hazifanywi kwenye majumba hayo aidha kwa kuwa wafanyibiasha wanahofia maisha au wateja hawapo. Amani ya ncho siyo udhabiti wa dhamani ya shilingi kule nje ilhali wenye shilingi hawauzi wala kununua chochote katika nchi yao kwa kuwa hakuna usalama. Amani ya nchi si kuwa na makabila mengi yenye utajiri lakini ambayo yanachochewa na kupigana wakati wowote. Hiyo si amani ya nchi.

Msimu wa uchaguzi nchini nafikiri ni wakati ambapo meli ya taifa letu huyumbayumba na kuwatia hofu mabaharia ambao ni wakenya. Mwaka huu tumeshuhudia mengi tu ; vifo, maandamano, uporaji kwa jina la kuandamana, mizungu ya Chiloba, mizungu ya Maraga, mizungu ya Matiang'i na karibuni, kombora la Akombe. Kenya inayumbayumba. Wakenya wasomi ambao tunatarajia wawe vielelezo wanatupiana sumu kwenye mitandao ya kijamii huku kila mmoja, kwa kusalitiwa na jina lake (chambilecho Mung'ou) anavuta ngozi akielekeza kwake. Wanyonge wasonge tuna wasiwasi mkubwa kuhusu kitakachotokea baada ya oktoba 26.

Tatizo kuu la mkenya ni kuwa hapendi kusoma. Ikiwa wakenya tungependa kusoma, basi vitabu vya fasihi vingetufunua akili na matatizo kama haya ya sasa tungeyaondoa zamani sana bila hata kumwaga damu. Kauli nyingi ambazo tunazitoa kwenye mitandao hazitukeji tu bali zinadhihirisha ufinyu wetu kimawazo na kibunifu. Utampata mtu anadai kuwa " VITU AMBAVYO SIWEZI KUPINGA MAISHANI : NENO LA MUNGU na NENO LA RAILA AU NENO LA MUNGU na MENO LA UHURU."  Kauli hizi huendana sawasawa  na miegemeo yetu kisiasa. Wengi tunaegemea kwa hawa MAKABAILA wawili kwa sababu majina yetu yanalandana. Lakini mbona umwabudu binadamu mwenzako ambaye leo yupo na kesho Kageuka upepo baada ya kufariki? Mbona umwabudu kiasi cha kumwua jirani yako, kabwela kama wewe ati kwa sababu yake? Tunahadaiwa mara nyingi kuwa wao wana uwezo wa kubadilisha hali yetu kimaisha. La! Tunadhani kuwa mwanasiasa ndiye atakayetatua shida zetu ilhali kwa kiasi fulani yeye ndiye anayesababisha maafa, na yeye hafi kwa jina la mabadiliko au demokrasia. Changamoto kubwa zaidi hasa ni kuwa, hata wanafunzi wa Vyuo vikuu wana fikira kama hizo. Wanabebewa akili! Mbona basi walienda shule? Kusema kuwa mtu fulani amesema na hivyo hupingi, kunaonyesha tu jinsi hatujitegemei kimawazo. Tunawaziwa. Tumegeuza wanasiasa hawa wawili kuwa Mungu wa pili, tunawaabudu kama nini. Lakini niwakumbushe kuwa wao hawafi kwa mtutu wala upanga. Benki zao zinatapika madola na mayuro. Familia zao zinajivunia mashamba makubwa makubwa, utajiri usiyomithilika na wanalindwa na polisi na nguvu zao za kishetani kila wakati. Wewe kifyefye, unayekula mihogo mikavu kwa maji unayoyapata kwa nadra, unachochewa dhidi ya jirani na kumwua. Ikiwa Mluo ni adui ya Mkikuyu, ninatarajia Raila Odinga ashike bunduki na kusafirisha risasi ndani ya kichwa cha Rais Uhuru Kenyatta. Ikiwa Mkalenjin ni Adui ya Mluo, ninatarajia Naibu Rais kuchukua mkuki na kumdunga Raila au Wetangula kwenye ini. Wao hawauwani, wanapigana tu kwa midomo. Sisi makabwela ndio vifaa vya kuwaua wakenya wenzetu. Ikiwa tunaiga, basi huku kuuana tunaiga kutoka kwa nani? Ikiwa tungekuwa tunawaiga, basi tungegombana mchana na usiku tunalala bila kumwaga damu. Nani mjinga? Kabaila au Kabwela? Ninaomba arobaini za hawa makabaila wawili ambao wameiteka Kenya tangu ipate uhuru zifike ili waondoke katika siasa. Nione sasa tutaabudu nani. BABA AKISEMA SIPINGI!

#soma makala ya Waraka kwa Wachochezi : bonyeza kidude cha HOMES kisha uchague cha kusoma. DUMISHENI AMANI 

1 comment: