Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Sunday, 14 January 2018

KITANDIKE KITANDA UBADILISHE DUNIA

Ni jambo dogo sana na ambalo watu wengi hawalitilii maanani. Walio katika ndoa huiwacha kazi hiyo ili wake zao waifanye ingawa natilia shaka ikiwa kweli mwanamke wa karne hii anaweza kufanya hivyo kwa niaba ya mumewe tangu kusawawazishwa kwa jinsia duniani. Katika utamaduni wa jamii yetu, kazi hiyo ni ya mwanamke. Kapera kifani changu huamka asubuhi na kukiacha kitanda bila kukitandika na kukitandaza vyema. Ingawa ni jambo dogo, shughuli hii kifasihi ina manufaa mengi mno.

Kwanza ni mwanzo wa usafi. Walisema wenye lugha, nyumba nzuri si mlango, fungua uingie ndani. Naam, ikiwa utakuwa nadhifu uendapo ofisini na kitanda chako si safi, usafi wako ni wa kutilia shaka. Mwanzo wa usafi wa siku ni kusafisha kitanda chako. Usikiache kikiwa kimevurugika kama utumbo wa mbuzi.

Pili, utakuwa umekamilisha shughuli ya kwanza ya siku. Hili litakupa ari ya kufanya shughuli nyinginezo hata ziwe ngumu kama miamba kwa kuwa umeishachochewa. Umechochewa kwa kukamilisha shughuli ya kwanza ya siku na kuonyesha mwanzo wa kuwajibika. Kumbuka siku njema, huanza asubuhi.

Tatu, kutandika kutaeleza jinsi unavyothamini mambo hata yawe madogo maishani. Kumbuka ikiwa hutafauli kukamilisha mambo madogo maishani, hata makubwa yatakushinda. Anayekithamini kitu kidogo mfano wa mbegu ya haradali, ana uwezo mkubwa wa kukamilisha jambo alianzalo hata liwe kubwa kama mkuyu. Kumbuka kuwa mwanzo wa ngoma ni lele.

Nne. Utajiondolea woga, uchoyo na ubinafsi. Ukitandika kitanda asubuhi, utakuwa umetenga nafasi ndogo moyoni mwako. Nafasi ya kumkaribisha yeyote, awe mgeni mashuhuri au mgeni tu mwako. Hutakuwa na woga wa kumkaribisha kwenye kitanda chako kwa kuwa ki safi. Kikiwaka na moshi utazuka.

Tano. Jioni utakuwa na jambo la kujifariji na kujiliwaza. 'hata ingawa nimeshindwa kuzikamilisha shughuli kuu za siku, aghalabu nina cha kujivunia siku hii. Nilikamilisha shughuli ya kwanza ya kutandika kitanda japo ndogo.'

Sita. Utajiepusha na visingizio na visababishi vya ugomvi katika nyumba. Mume aliyejaa hasira  kutokana na siku kuwa mbaya, huweza kutafuta visingizio vidogo vidogo ili apunguze hasira zake kwa kumchapa mkewe. Hili jambo dogo la kutokutandika kitanda huenda likawa kisingizio. kitandike kitanda kabla. Kumbuka aliyekando haangukiwi na mti.

Saba. utarahisishiwa kazi jioni ujapo. Fikiria urejee nyumbani jioni ukiwa na fadhaa. Kisha ukipate kitanda, ambacho huwa ni kitulizo wakati mwingine, kiwe kimevurugika. Au utoke kazini ukiwa umechoka tiki. Ikiwa hukuwa imekitandika kitanda, utaongeza mfadhaiko moyoni kwa kutakiwa kukitandika ndipo ulale. Kumbuka kazi hiyo ndogo pia yaweza chosha kwa mtu aliyerejea akiwa kachoka tayari. Maji ya kifuu, bahari ya chungu.

Nane. Uendapo mapumzikoni usiku baada ya shughuli za siku na upate kitanda chako kikiwa kimetandazwa, utakuwa na matumaini kuwa utalala vizuri, utakuwa na njozi njema na inshallah siku mpya itakuwa ya mafanikio. Rasharasha ndiyo mwanzo wa mvua.

Anayetaka kubadilisha dunia ilhali hakitandiki kitanda chake asome haya : HUNA MSHIPI, HUNA NGWE, KUOMOA TENGA NI NINI? Tandika kitanda ubadilishe dunia


@Tungo za Daniel Si'wa (fb)

No comments:

Post a Comment