Mefika na simulizi,
Sikilizeni hadithi,
Ya mja mtanashati,
Aliyekwenda mbinguni,
Dunia alikoishi,
Hakuelewa mapenzi,
Aliteswa kwa matani,
Ha'tulia asilani,
Aliwachumbia wengi,
Ila hakuwadhibiti,
Walimponyoka.
Akaikata shauri,
Amzuru mwenyezi,
Kwa kuwa aliamini,
yeye ndiye muumbaji,
Wa mizungu ya mapenzi,
Alijawa na maswali,
Ya kumwuliza mwenyezi,
Kubwa likiwa ni hili,
Aelezewe abaini,
Huba yamaanishani?
Aliwachumbia wengi,
Ila hakuwadhibiti,
Walimponyoka!
"Nakutuma msituni,
Ulichume ua zuri,
La weupe wa katani,
Livutialo kwa rihi,
Lipendezalo machoni,
Litulizalo moyoni,
Kileta mtanashati,
taeleza ubaini,
Hasa ni nini mapenzi,"
Aliwachumbia wengi,
Ila hakuwadhibiti,
Walimponyoka!
Akafuata vichochoroni,
Akitafuta ua zuri,
La kupendeza moyoni,
Aliyapita tu mengi,
Ya manjano na hudhurungi,
Aliyapita ya samawati,
Na yaliyokoza ujani,
Jekundu likamuwini,
Urembo wake ukaafiki,
Ila akenda ndani,
Atafute la ulimbo zaidi,
Katembea hatua nyingi,
Hadi kule tamati,
Hakupata la kuafiki,
La kumteka moyoni,
Akarejelea la awali,
Hakulipata asilani,
Lilipendeza sana wengi,
Wakalitwaa wa ujasiri,
Wenye mapenzi nyoyoni,
Akarejea mbinguni,
Akiwa hana hanani,
Aliwachumbia wengi,
Ila hakuwadhibiti,
Walimponyoka!
"Li wapi ua ndugu,
Lilokutuma kwenye msitu?"
"Samahani mwenyezi mungu,
Lipata kufu yangu,
Ila kazama kwenye msitu,
Kutafuta lisilo mafutu,
Ila zikawa sulubu,
Sikujua ninakufuru,
Lirejea kwenye kichungu,
Walishachuma wa machungu, "
Hayo sasa ndo' mahaba,
Ukiwa naye wamshiba,
Wamchezea shengesha,
Na za chini kayaya,
Pindi ukishampoteza,
Mwingine hutampata,
Kifani cha zake tabia,
Penzi ukiumba,
Usiwe wa kuumbua,
Mke nguo bomba,
Mgomba hupaliliwa,
Mume la koko tunda,
Halidari bahari hata!
Aliwachumbia wengi,
Ila hakuwadhibiti,
Walimponyoka!

No comments:
Post a Comment