Featured post

KASISI FISADI : LUSAKA AZOMEWA BUNGOMA

 Wanyeji wa Bungoma wamemkemea Gavana wa Jimbo hilo Kenneth Makelo Lusaka. Katika maoni waliyotoa mtandaoni, wananchi wamempaka samli ya ufi...

Friday, 8 June 2018

RISALA KWA DADA ANYANGO



Umetupa mushituko, habari tulipopata,
Kimekuchukua kifo, hata bila kukupasha,
Kwa muda huo mdogo, Anyango usingeaga,
Salama dada Anyango, ulale pema ahera.

Kingekuwa masikio, kisikuje ngekiomba,
Au kiwa na mdomo, ujipange kingesema,
Ungekiona kwa macho, ama  ungekitoroka,
Salama dada Anyango, ulale pema ahera

Walia marafikizo, kwa huzuni ulowapa,
Walia wazazi wako, kwa vile umewaacha,
Twalia nasi wenzako, kwa pengo uliloacha,
Salama dada Anyango, ulale pema ahera.

Tunajawa na kitapo, jenezani ukilala,
Ukienda jongomeo, tunadhani tunaota,
Kilio kisokikomo, kwa marafiki na jama,
Salama dada Anyango, ulale pema ahera.

Tazama kitanda chako, nani atakilalia,
Na hiyo nafasi yako, nani ataichukua,
Hizo nguo nzuri zako, ni nani atazivaa,
Salama dada Anyango, ulale pema ahera.

Kakamega ni kilio, ulokuwa mwanachama,
COWESA pia kilio, jamani itakupeza,
Bungoma Busia Kihoro, Vihiga pia walia,
Salama dada Anyango, ulale pema ahera.

Hatutapata kikoko, kwa donda uliloacha,
Kwetu wewe si mapeto, tukusahau haraka,
Utabakia mioyo, kwenye kiti cha mtima,
Salama dada Anyango, ulale pema ahera

Dunia kweli mapito, twapita zetu twaenda,
Milima aridhi mito, ndiyo itayosalia,
Binadamu ni upepo, apita huku kivuma,
Salama dada Anyango, ulale pema ahera,

@Daniel Kaka Si'wa


No comments:

Post a Comment